Israeli Asiye Na Toba
1“Njooni, tumrudie Bwana.
Ameturarua vipande vipande
lakini atatuponya;
ametujeruhi lakini
atatufunga majeraha yetu.
2Baada ya siku mbili atatufufua;
katika siku ya tatu atatuinua,
ili tuweze kuishi mbele zake.
3Tumkubali Bwana,
tukaze kumkubali yeye.
Kutokea kwake ni hakika kama vile
kuchomoza kwa jua;
atatujia kama mvua za masika,
kama vile mvua za vuli
ziinyweshavyo nchi.”
4“Nifanye nini nawe, Efraimu?
Nifanye nini nawe, Yuda?
Upendo wako ni kama ukungu wa asubuhi,
kama umande wa alfajiri utowekao.
5Kwa hiyo ninawakata ninyi vipande vipande
kwa kutumia manabii wangu;
nimewaua ninyi kwa maneno ya kinywa changu,
hukumu zangu zinawaka
kama umeme juu yenu.
6Kwa maana nataka rehema, wala si dhabihu,
kumkubali Mungu zaidi
kuliko sadaka za kuteketezwa.
7Wamevunja Agano kama Adamu:
huko hawakuwa waaminifu kwangu.
8Gileadi ni mji wenye watu waovu,
umetiwa madoa kwa nyayo za damu.
9Kama wanyangʼanyi wamviziavyo mtu,
ndivyo magenge ya makuhani wafanyavyo;
wanaulia watu kwenye njia iendayo Shekemu,
wakifanya uhalifu wa aibu.
10Nimeona jambo la kutisha
katika nyumba ya Israeli.
Huko Efraimu amejitolea kwa ukahaba
na Israeli amenajisika.
11“Pia kwa ajili yako, Yuda,
mavuno yameamriwa.
“Wakati wowote ningerejesha neema ya watu wangu,