Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno) 2015

Isaya 1:1-31

1Maono kuhusu Yuda na Yerusalemu ambayo Isaya mwana wa Amozi aliyaona wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.

Taifa Asi

2Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia!

Kwa maana Bwana amesema:

“Nimewalisha watoto na kuwalea,

lakini wameniasi mimi.

3Ngʼombe anamjua bwana wake,

naye punda anajua hori la mmiliki wake,

lakini Israeli hajui,

watu wangu hawaelewi.”

4Lo! Taifa lenye dhambi,

watu waliolemewa na uovu,

uzao wa watenda mabaya,

watoto waliozoelea upotovu!

Wamemwacha Bwana,

Wamemkataa kwa dharau

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli

na kumgeuzia kisogo.

5Kwa nini mzidi kupigwa?

Kwa nini kudumu katika uasi?

Kichwa chako chote kimejeruhiwa,

moyo wako wote ni mgonjwa.

6Kutoka wayo wako wa mguu hadi kwenye utosi wa kichwa chako

hakuna uzima:

ni majeraha matupu na makovu

na vidonda vitokavyo damu,

havikusafishwa au kufungwa

wala kulainishwa kwa mafuta.

7Nchi yenu imekuwa ukiwa,

miji yenu imeteketezwa kwa moto;

nchi yenu imeachwa tupu na wageni

mbele ya macho yenu,

imeharibiwa kama vile imepinduliwa na wageni.

8Binti Sayuni ameachwa kama kipenu

katika shamba la mizabibu,

kama kibanda katika shamba la matikitimaji,

kama mji uliohusuriwa.

9Kama Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote1:9 Bwana Mwenye Nguvu Zote hapa ni Yehova Sabaoth, yaani Bwana wa Majeshi; pia Warumi 9:29 na Yakobo 5:4.

asingelituachia walionusurika,

tungelikuwa kama Sodoma,

tungelifanana na Gomora.

10Sikieni neno la Bwana,

ninyi watawala wa Sodoma;

sikilizeni sheria ya Mungu wetu,

enyi watu wa Gomora!

11Bwana anasema, “Wingi wa sadaka zenu,

ni kitu gani kwangu?

Ninazo sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi,

za kondoo dume na mafuta ya wanyama walionona.

Sipendezwi na damu za mafahali

wala za wana-kondoo na mbuzi.

12Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu,

ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo,

huku kuzikanyaga nyua zangu?

13Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana!

Uvumba wenu ni chukizo kwangu.

Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada:

siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.

14Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa:

moyo wangu unazichukia.

Zimekuwa mzigo kwangu,

nimechoka kuzivumilia.

15Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi,

nitaficha macho yangu nisiwaone;

hata mkiomba maombi mengi

sitasikiliza.

Mikono yenu imejaa damu;

16jiosheni na mkajitakase.

Yaondoeni matendo yenu maovu

mbele zangu!

Acheni kutenda mabaya,

17jifunzeni kutenda mema!

Tafuteni haki,

watieni moyo walioonewa.

Teteeni shauri la yatima,

wateteeni wajane.

18“Njooni basi tuhojiane,”

asema Bwana.

“Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,

zitakuwa nyeupe kama theluji;

ingawa ni nyekundu sana kama damu,

zitakuwa nyeupe kama sufu.

19Kama mkikubali na kutii,

mtakula mema ya nchi,

20lakini kama mkikataa na kuasi,

mtaangamizwa kwa upanga.”

Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena.

21Tazama jinsi mji uliokuwa mwaminifu

umekuwa kahaba!

Mwanzoni ulikuwa umejaa unyofu,

haki ilikuwa inakaa ndani yake,

lakini sasa ni wauaji!

22Fedha yenu imekuwa takataka,

divai yenu nzuri imechanganywa na maji.

23Watawala wenu ni waasi,

rafiki wa wevi,

wote wanapenda rushwa

na kukimbilia hongo.

Hawatetei yatima,

shauri la mjane haliletwi mbele yao lisikilizwe.

24Kwa hiyo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote,

Mwenye Nguvu wa Israeli, asema hivi:

“Lo, nitapata faraja kutoka kwa adui zangu

na kujilipizia kisasi juu ya watesi wangu.

25Nitauelekeza mkono wangu dhidi yenu,

nitawasafisha takataka zenu zote

na kuwaondolea unajisi wenu wote.

26Nitawarudishia waamuzi wenu kama ilivyokuwa siku za zamani,

nao washauri wenu kama ilivyokuwa mwanzoni.

Baadaye utaitwa,

Mji wa Haki,

Mji Mwaminifu.”

27Sayuni itakombolewa kwa haki,

wale waliomo ndani yake waliotubu kwa uaminifu.

28Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa,

nao wanaomwacha Bwana wataangamia.

29“Mtaaibika kwa sababu ya hiyo mialoni

ambayo mlifurahia,

mtafadhaika kwa sababu ya bustani

mlizozichagua.

30Mtakuwa kama mwaloni wenye majani yanayonyauka,

kama bustani isiyokuwa na maji.

31Mtu mwenye nguvu atatoweka kama majani makavu yawakayo moto,

na kazi yake kama cheche ya moto;

vyote vitaungua pamoja,

wala hakuna wa kuuzima huo moto.”