Kuzaliwa Kwa Yesu
(Mathayo 1:18-25)
1Siku zile Kaisari Augusto alitoa amri kwamba watu wote waandikishwe katika ulimwengu wa Kirumi. 2(Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyofanyika wakati Krenio alikuwa mtawala wa Shamu2:2 Shamu inamaanisha Syria.). 3Kila mtu alikwenda kuandikishwa katika mji wake alikozaliwa.
4Hivyo Yosefu akapanda kutoka mji wa Nazareti ulioko Galilaya kwenda Uyahudi, mpaka Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi. 5Alikwenda huko kujiandikisha pamoja na Maria, ambaye alikuwa amemposa naye alikuwa mjamzito. 6Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Maria wa kujifungua ukawa umetimia, 7naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori ya kulia ngʼombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni.
Wachungaji Na Malaika
8Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. 9Ghafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawangʼaria kotekote, wakaingiwa na hofu. 10Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote. 11Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo2:11 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. Bwana. 12Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori ya kulia ngʼombe.”
13Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema,
14“Atukuzwe Mungu juu mbinguni,
na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”
15Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya ya ajabu yaliyotukia, ambayo Bwana ametuambia habari zake.”
16Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ngʼombe. 17Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyo mtoto. 18Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo. 19Lakini Maria akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari. 20Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona.
21Hata zilipotimia siku nane, ulikuwa ndio wakati wa kumtahiri mtoto, akaitwa Yesu, jina alilokuwa amepewa na malaika kabla hajatungwa mimba.
Yesu Apelekwa Hekaluni
22Ulipotimia wakati wa utakaso wake Maria kwa mujibu wa Sheria ya Mose, basi Yosefu na Maria walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Bwana 23(kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Bwana”), 24na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Sheria ya Bwana: “Hua wawili au makinda mawili ya njiwa.”
25Basi alikuwako huko Yerusalemu mtu mmoja jina lake Simeoni, ambaye alikuwa mwenye haki na mcha Mungu, akitarajia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. 26Roho Mtakatifu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Kristo wa Bwana. 27Simeoni, akiwa ameongozwa na Roho Mtakatifu, alikwenda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Yesu ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Sheria, 28ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema:
29“Bwana Mwenyezi, kama ulivyoahidi,
sasa wamruhusu mtumishi wako
aende zake kwa amani.
30Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako,
31ulioweka tayari machoni pa watu wote,
32nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa
na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.”
33Naye Yosefu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto. 34Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, “Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake, 35ili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike. Nao upanga utauchoma moyo wako.”
36Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa. 37Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na minne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba. 38Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu.
39Yosefu na Maria walipokuwa wamekamilisha mambo yote yaliyotakiwa na Sheria ya Bwana, walirudi mjini kwao Nazareti huko Galilaya. 40Naye yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu, akiwa amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
Kijana Yesu Hekaluni
41Kila mwaka Yosefu na Maria mama yake Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka. 42Yesu alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, walipanda kwenda kwenye Sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. 43Baada ya Sikukuu kumalizika, wakati Yosefu na Maria mama yake walipokuwa wakirudi nyumbani, Yesu alibaki Yerusalemu lakini hawakutambua. 44Wao wakidhani kuwa yuko miongoni mwa wasafiri, walienda mwendo wa kutwa nzima. Ndipo wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa zao na marafiki. 45Walipomkosa walirudi Yerusalemu ili kumtafuta. 46Baada ya siku tatu wakamkuta ndani ya Hekalu, akiwa ameketi katikati ya walimu wa sheria, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47Wote waliomsikia walistaajabishwa na uwezo wake mkubwa wa kuelewa, na majibu aliyoyatoa. 48Yosefu na Maria mama yake walipomwona walishangaa. Mama yake akamuuliza, “Mwanangu, mbona umetufanyia hivi? Tazama, mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta kwa wasiwasi mkubwa kila mahali.”
49Yesu akawaambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua kwamba imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?”
50Lakini wao hawakuelewa maana ya lile alilowaambia.
51Ndipo akashuka pamoja nao hadi Nazareti, naye alikuwa mtiifu kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote. 52Naye Yesu akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.