Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno) 2015

Marko 3:1-35

Mtu Aliyepooza Mkono Aponywa

(Mathayo 12:9-14; Luka 6:6-11)

1Yesu akaingia tena ndani ya sinagogi, na huko palikuwa na mtu aliyepooza mkono. 2Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki. 3Yesu akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele ya watu wote.”

4Kisha Yesu akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato: Ni kutenda mema au kutenda mabaya? Ni kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza kimya.

5Yesu akawatazama pande zote kwa hasira, akahuzunika sana kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa kabisa! 6Kisha Mafarisayo wakatoka nje, nao wakaanza kufanya shauri la kumuua Yesu wakiwa na Maherode.

Umati Wa Watu Wamfuata Yesu

7Yesu pamoja na wanafunzi wake wakaondoka huko wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya ukamfuata. 8Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, umati mkubwa wa watu ukamjia kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumaya, na ngʼambo ya Yordani, pamoja na wale wa sehemu za karibu na Tiro na Sidoni. 9Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake waweke tayari mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga. 10Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa. 11Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.” 12Lakini aliwaonya wasimseme yeye ni nani.

Yesu Achagua Mitume Kumi Na Wawili

(Mathayo 10:1-4; Luka 6:12-16)

13Yesu akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia. 14Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume, ili wapate kuwa pamoja naye, na awatume kwenda kuhubiri 15na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu. 16Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua: Simoni (ambaye alimwita Petro); 17Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo); 18Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomaso, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo, 19na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.

Yesu Na Beelzebuli

(Mathayo 12:22-32; Luka 11:14-23; 12:10)

20Kisha Yesu aliporudi nyumbani, umati wa watu ukakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula. 21Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”

22Walimu wa sheria walioteremka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli!3:22 Beelzebuli kwa Kiyunani ni Beelzebubu, yaani mkuu wa pepo wachafu. Anatoa pepo wachafu kwa kutumia mkuu wa pepo wachafu!”

23Basi Yesu akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani? 24Kama ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama. 25Nayo nyumba kama ikigawanyika dhidi yake yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama. 26Naye Shetani kama akijipinga mwenyewe na awe amegawanyika, hawezi kusimama bali mwisho wake umewadia. 27Hakuna mtu yeyote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu. Ndipo ataweza kuteka nyara mali zake. 28Amin, nawaambia, dhambi zote na makufuru yote ya wanadamu watasamehewa. 29Lakini yeyote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”

30Yesu alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”

Mama Na Ndugu Zake Yesu

(Mathayo 12:46-50; Luka 8:19-21)

31Kisha wakaja ndugu zake Yesu pamoja na mama yake. Wakasimama nje, wakamtuma mtu kumwita. 32Umati wa watu ulikuwa umeketi kumzunguka, nao wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”

33Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”

34Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu. 35Mtu yeyote anayetenda mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na dada yangu na mama yangu.”