Mtawala Aliyeahidiwa Kutoka Bethlehemu
1Panga majeshi yako, ee mji wa majeshi,
kwa kuwa kuzingirwa kumepangwa dhidi yetu.
Watampiga mtawala wa Israeli
shavuni kwa fimbo.
2“Lakini wewe, Bethlehemu Efrathi,
ingawa u mdogo miongoni mwa koo za Yuda,
kutoka kwako atatokea kwa ajili yangu
yeye atakayekuwa mtawala katika Israeli,
ambaye asili yake ni kutoka zamani,
kutoka milele.”
3Kwa hiyo Israeli utaachwa mpaka wakati
mwanamke aliye na utungu atakapozaa
na ndugu zake wengine warudi
kujiunga na Waisraeli.
4Atasimama na kulichunga kundi lake
katika nguvu ya Bwana,
katika utukufu wa jina la Bwana Mungu wake.
Nao wataishi kwa usalama, kwa kuwa wakati huo
ukuu wake utaenea hadi miisho ya dunia.
5Naye atakuwa amani yao.
Ukombozi Na Uharibifu
Wakati Mwashuru atakapovamia nchi yetu
na kupita katika ngome zetu,
tutawainua wachungaji saba dhidi yake,
hata viongozi wanane wa watu.
6Wataitawala nchi ya Ashuru kwa upanga,
nchi ya Nimrodi kwa upanga.
Atatuokoa kutoka kwa Mwashuru
atakapoivamia nchi yetu
na kuingia katika mipaka yetu.
7Mabaki ya Yakobo yatakuwa
katikati ya mataifa mengi
kama umande kutoka kwa Bwana,
kama manyunyu juu ya majani,
ambayo hayamngoji mtu
wala kukawia kwa mwanadamu.
8Mabaki ya Yakobo yatakuwa miongoni mwa mataifa,
katikati ya mataifa mengi,
kama simba miongoni mwa wanyama wa msituni,
kama mwana simba miongoni
mwa makundi ya kondoo,
ambaye anaumiza vibaya na kuwararua
kila anapopita katikati yao,
wala hakuna awezaye kuokoa.
9Mkono wako utainuliwa juu kwa ushindi juu ya watesi wako,
nao adui zako wote wataangamizwa.
10“Katika siku ile,” asema Bwana,
“nitaangamiza farasi zenu katikati yenu
na kubomoa magari yenu ya vita.
11Nitaiangamiza miji ya nchi yenu
na kuziangusha chini ngome zenu zote.
12Nitaangamiza uchawi wenu
na hamtapiga tena ramli.
13Nitaangamiza vinyago vyenu vya kuchonga
na mawe yenu ya ibada yatoke katikati yenu;
hamtasujudia tena
kazi ya mikono yenu.
14Nitangʼoa nguzo za Ashera katikati yenu
na kubomoa miji yenu.
15Nitalipiza kisasi kwa hasira na ghadhabu
juu ya mataifa ambayo hayajanitii.”