Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno) 2015

Nahumu 3:1-19

Ole Wa Ninawi

1Ole wa mji umwagao damu,

uliojaa uongo,

umejaa nyara,

usiokosa kuwa na vitu vya kuteka nyara.

2Kelele za mijeledi,

vishindo vya magurudumu,

farasi waendao mbio

na mshtuo wa magari ya vita!

3Wapanda farasi wanaenda mbio,

panga zinameremeta,

na mikuki inangʼaa!

Majeruhi wengi,

malundo ya maiti,

idadi kubwa ya miili isiyohesabika,

watu wanajikwaa juu ya mizoga:

4yote haya kwa sababu ya wingi wa tamaa za kahaba,

anayeshawishi, bibi wa mambo ya uchawi,

anayewatia utumwani mataifa kwa ukahaba wake

na pia jamaa za watu kwa ulozi wake.

5Bwana Mwenye Nguvu Zote anasema,

“Mimi ni kinyume na ninyi.

Nitafunika uso wako kwa gauni lako.

Nitaonyesha mataifa uchi wako

na falme aibu yako.

6Nitakutupia uchafu,

nitakufanyia dharau

na kukufanya kioja.

7Wote wanaokuona watakukimbia na kusema,

‘Ninawi ipo katika kuangamia:

ni nani atakayeomboleza kwa ajili yake?’

Nitampata wapi yeyote wa kukufariji?”

8Je, wewe ni bora kuliko No-Amoni,

uliopo katika Mto Naili,

uliozungukwa na maji?

Mto ulikuwa kinga yake,

nayo maji yalikuwa ukuta wake.

9Kushi3:9 Kushi ni Ethiopia. na Misri walikuwa nguvu zake zisizo na mpaka;

Putu na Libia walikuwa miongoni mwa wale walioungana naye.

10Hata hivyo alichukuliwa mateka

na kwenda uhamishoni.

Watoto wake wachanga walivunjwa vunjwa vipande

kwenye mwanzo wa kila barabara.

Kura zilipigwa kwa watu wake wenye heshima,

na watu wake wote wakuu walifungwa kwa minyororo.

11Wewe pia utalewa;

utakwenda mafichoni

na kutafuta kimbilio kutoka kwa adui.

12Ngome zako zote ni kama mitini

yenye matunda yake ya kwanza yaliyoiva;

wakati inapotikiswa,

tini huanguka kwenye kinywa chake alaye.

13Tazama vikosi vyako:

wote ni wanawake!

Malango ya nchi yako

yamekuwa wazi kwa adui zako;

moto umeteketeza mapingo yake.

14Teka maji kwa ajili ya kuzingirwa kwako,

imarisha ulinzi wako,

Ufanyie udongo wa mfinyanzi kazi,

yakanyage matope,

karabati tanuru la kuchomea matofali!

15Huko moto utakuteketeza,

huko upanga utakuangusha chini

na kama vile panzi, watakumaliza.

Ongezeka kama panzi,

ongezeka kama nzige!

16Umeongeza idadi ya wafanyabiashara wako

mpaka wamekuwa wengi kuliko nyota za angani,

lakini kama nzige wanaacha nchi tupu

kisha huruka na kwenda zake.

17Walinzi wako ni kama nzige,

maafisa wako ni kama makundi ya nzige

watuao kwenye kuta wakati wa siku ya baridi:

lakini wakati jua linapotokea wanaruka kwenda zao,

na hakuna ajuaye waendako.

18Ee mfalme wa Ashuru, wachungaji wako wanasinzia;

wakuu wako wanalala chini mavumbini kupumzika.

Watu wako wametawanyika juu ya milima

bila kuwa na mtu yeyote wa kuwakusanya.

19Hakuna kitu kinachoweza kuponya jeraha lako;

jeraha lako ni la kukuua.

Kila anayesikia habari zako,

hupiga makofi kwa kuanguka kwako,

kwa kuwa ni nani ambaye hajaguswa

na ukatili wako usio na mwisho?