Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno) 2015

Sefania 1:1-18

1Neno la Bwana lililomjia Sefania mwana wa Kushi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hezekia, wakati wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda:

Onyo La Maangamizi Yanayokuja

2Bwana asema,

“Nitafagia kila kitu

kutoka kwenye uso wa dunia.”

3“Nitafagilia mbali watu na wanyama;

nitafagilia mbali ndege wa angani

na samaki wa baharini.

Wafanyao maovu watapata tu kokoto,

nami nitamkatilia mbali mwanadamu atoke katika dunia,”

asema Bwana.

Dhidi Ya Yuda

4“Nitaiadhibu Yuda

na wote wakaao Yerusalemu.

Kutoka mahali hapa nitakatilia mbali

kila mabaki ya Baali,

majina ya wapagani na makuhani

waabuduo sanamu:

5wale ambao husujudu juu ya mapaa

kuabudu jeshi la vitu vya angani,

wale ambao husujudu na kuapa kwa Bwana

na ambao pia huapa kwa Malkamu,

6wale wanaoacha kumfuata Bwana,

wala hawamtafuti Bwana

wala kutaka shauri lake.

7Nyamazeni mbele za Bwana Mwenyezi,

kwa maana siku ya Bwana iko karibu.

Bwana ameandaa dhabihu,

amewaweka wakfu wale aliowaalika.

8Katika siku ya dhabihu ya Bwana

nitawaadhibu wakuu

na wana wa mfalme

na wale wote wanaovaa

nguo za kigeni.

9Katika siku hiyo nitaadhibu wote ambao

hukwepa kukanyaga kizingiti,

ambao hujaza hekalu la miungu yao

kwa dhuluma na udanganyifu.”

10Bwana asema, “Katika siku hiyo

kilio kitapanda juu kutoka lango la Samaki,

maombolezo kutoka mtaa wa pili,

na mshindo mkubwa kutoka vilimani.

11Ombolezeni, ninyi mnaoishi katika eneo la sokoni;

wafanyabiashara wenu wote wameangamizwa,

wote ambao wanafanya biashara ya fedha

wataangamizwa.

12Wakati huo nitasaka mji wa Yerusalemu kwa taa,

na kuwaadhibu wale ambao

wanakaa katika hali ya kuridhika,

ambao ni kama divai

iliyobaki kwenye machicha,

ambao hudhani, ‘Bwana hatafanya lolote,

jema au baya.’

13Utajiri wao utatekwa nyara,

nyumba zao zitabomolewa.

Watajenga nyumba,

lakini hawataishi ndani yake;

watapanda mizabibu

lakini hawatakunywa divai yake.

Siku Kubwa Ya Bwana

14“Siku kubwa ya Bwana iko karibu:

iko karibu na inakuja haraka.

Sikilizeni! Kilio katika siku ya Bwana

kitakuwa kichungu,

hata shujaa atapiga kelele.

15Siku ile ni siku ya ghadhabu,

siku ya fadhaa na dhiki,

siku ya uharibifu na ukiwa,

siku ya giza na utusitusi,

siku ya mawingu na giza nene,

16siku ya tarumbeta na mlio wa vita

dhidi ya miji yenye ngome

na dhidi ya minara mirefu.

17Nitawaletea watu dhiki,

nao watatembea kama vipofu,

kwa sababu wametenda dhambi

dhidi ya Bwana.

Damu yao itamwagwa kama vumbi

na matumbo yao kama taka.

18Fedha yao wala dhahabu yao

hazitaweza kuwaokoa

katika siku hiyo ya ghadhabu ya Bwana.

Katika moto wa wivu wake

dunia yote itateketezwa,

kwa maana ataleta mwisho

wa wote wanaoishi katika dunia ghafula.”