Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno) 2015

Sefania 2:1-15

1Kusanyikeni pamoja, kusanyikeni pamoja,

enyi taifa lisilo na aibu,

2kabla ya wakati ulioamriwa haujafika

na siku ile inayopeperusha kama makapi,

kabla hasira kali ya Bwana haijaja juu yenu,

kabla siku ya ghadhabu ya Bwana

haijaja juu yenu.

3Mtafuteni Bwana, enyi nyote wanyenyekevu wa nchi,

ninyi ambao hufanya lile analoamuru.

Tafuteni haki, tafuteni unyenyekevu;

labda mtahifadhiwa

siku ya hasira ya Bwana.

Dhidi Ya Ufilisti

4Gaza utaachwa

na Ashkeloni utaachwa magofu.

Wakati wa adhuhuri Ashdodi utaachwa mtupu

na Ekroni utangʼolewa.

5Ole wenu ninyi ambao mnaishi kando ya bahari,

enyi Wakerethi;

neno la Bwana liko dhidi yenu,

ee Kanaani, nchi ya Wafilisti.

“Mimi nitawaangamiza,

na hakuna atakayebaki.”

6Nchi kando ya bahari, mahali ambapo wanaishi Wakerethi,

patakuwa mahali pa wachungaji

na mazizi ya kondoo.

7Itakuwa mali ya mabaki ya nyumba ya Yuda,

hapo watapata malisho.

Wakati wa jioni watajilaza chini

katika nyumba za Ashkeloni.

Bwana Mungu wao atawatunza,

naye atawarudishia wafungwa wao.

Dhidi Ya Moabu Na Amoni

8“Nimeyasikia matukano ya Moabu

nazo dhihaka za Waamoni,

ambao waliwatukana watu wangu

na kutoa vitisho dhidi ya nchi yao.

9Hakika, kama niishivyo,”

asema Bwana Mwenye Nguvu Zote,

Mungu wa Israeli,

“hakika Moabu itakuwa kama Sodoma,

Waamoni kama Gomora:

mahali pa magugu na mashimo ya chumvi,

nchi ya ukiwa milele.

Mabaki ya watu wangu watawateka nyara;

mabaki ya taifa langu watarithi nchi yao.”

10Hiki ndicho watarudishiwa kwa ajili ya kiburi chao,

kwa kutukana na kudhihaki

watu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote.

11Bwana atakuwa wa kuhofisha kwao

atakapoangamiza miungu yote ya nchi.

Mataifa katika kila pwani yatamwabudu,

kila moja katika nchi yake.

Dhidi Ya Kushi

12“Ninyi pia, ee Wakushi,

mtauawa kwa upanga wangu.”

Dhidi Ya Ashuru

13Mungu atanyoosha mkono wake dhidi ya kaskazini

na kuangamiza Waashuru,

akiiacha Ninawi ukiwa

na pakame kama jangwa.

14Makundi ya kondoo na ngʼombe yatajilaza pale,

viumbe vya kila aina.

Bundi wa jangwani na bundi waliao kwa sauti nyembamba

wataishi juu ya nguzo zake.

Mwangwi wa kuita kwao utapita madirishani,

kifusi kitakuwa milangoni,

boriti za mierezi zitaachwa wazi.

15Huu ndio mji uliotukuka na kuishi kwa furaha

wakijisikia salama.

Ulisema moyoni mwako,

“Mimi ndimi, na wala hapana mwingine ila mimi.”

Jinsi gani umekuwa gofu,

mahali pa kulala wanyama pori!

Wote wanaopita kando yake wanauzomea

na kutikisa mkono kwa dharau.