Huduma Ya Paulo Kwa Watu Wa Mataifa
1Kwa sababu hii, mimi Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi watu wa Mataifa:
2Kwa hakika mmekwisha kusikia kuhusu ile huduma ya neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu, 3yaani, ile siri iliodhihirishwa kwangu kwa njia ya ufunuo, kama nilivyotangulia kuandika kwa kifupi. 4Kwa kusoma haya, basi mtaweza kuelewa ufahamu wangu katika siri ya Kristo. 5Siri hii haikudhihirishwa kwa wanadamu katika vizazi vingine kama vile sasa ilivyodhihirishwa na Roho kwa mitume na manabii watakatifu wa Mungu. 6Siri hii ni kwamba, kwa njia ya Injili, watu wa Mataifa ni warithi pamoja na Israeli, viungo vya mwili mmoja na washiriki pamoja wa ahadi katika Kristo Yesu.
7Nimekuwa mtumishi wa Injili hii kwa kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa nguvu yake itendayo kazi. 8Ingawa mimi ni mdogo kuliko aliye mdogo kabisa miongoni mwa watakatifu wote, nilipewa neema hii: ili niwahubirie watu wa Mataifa kuhusu utajiri usiopimika ulio ndani ya Kristo, 9na kuweka wazi kwa kila mtu siri hii iliyokuwa imefichwa tangu zamani katika Mungu, aliyeumba vitu vyote. 10Ili sasa kwa njia ya Kanisa, hekima yote ya Mungu ipate kujulikana kwa watawala na wenye mamlaka katika ulimwengu wa roho, 11sawasawa na kusudi lake la milele katika Kristo Yesu Bwana wetu. 12Ndani yake na kwa njia ya imani katika yeye twaweza kumkaribia Mungu kwa uhuru na kwa ujasiri. 13Kwa hiyo, nawaomba msikate tamaa kwa sababu ya mateso yangu kwa ajili yenu, hayo ni utukufu wenu.
Maombi Ya Paulo Kwa Waefeso
14Kwa sababu hii nampigia Baba magoti, 15ambaye ubaba wote wa kila jamaa za mbinguni na za duniani unatokana naye. 16Namwomba Mungu awaimarishe kwa kuwatia nguvu mioyo yenu kwa njia ya Roho wake kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, 17ili kwamba, Kristo apate kukaa mioyoni mwenu kwa njia ya imani. Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, 18mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, 19na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu.
20Basi kwa yeye awezaye kutenda mambo ya ajabu yasiyopimika kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya uweza wake ule utendao kazi ndani yetu, 21yeye atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kwa vizazi vyote, milele na milele. Amen.