Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno) 2015

Waefeso 4:1-32

Umoja Katika Mwili Wa Kristo

1Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa. 2Kwa unyenyekevu wote na upole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. 3Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani. 4Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja. 5Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja, 6Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote.

7Lakini kila mmoja wetu amepewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa cha Kristo. 8Kwa hiyo husema:

“Alipopaa juu zaidi, 4:8 Juu zaidi hapa ina maana mbingu za mbingu.

aliteka mateka,

akawapa wanadamu vipawa.”

9(Asemapo “alipaa juu,” maana yake nini isipokuwa ni kusema pia kwamba Kristo alishuka pande za chini sana za dunia?4:9 Pande za chini sana za dunia hapa maana yake Sheol kwa Kiebrania, yaani Kuzimu. 10Yeye aliyeshuka ndiye alipaa juu zaidi kupita mbingu zote, ili apate kuujaza ulimwengu wote.) 11Ndiye aliweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.

14Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

Maisha Ya Zamani Na Maisha Mapya

17Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu wa Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao. 18Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao. 19Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.

20Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyojifunza Kristo. 21Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu. 22Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu, 23ili mfanywe upya roho na nia zenu, 24mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.

Kanuni Za Maisha Mapya

25Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja. 26Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika, 27wala msimpe ibilisi nafasi. 28Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.

29Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao. 30Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwake mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. 31Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32Kuweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.