Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno) 2015

Yeremia 4:1-31

1“Ikiwa utataka kurudi, ee Israeli,

nirudie mimi,”

asema Bwana.

“Ikiwa utaondoa sanamu zako za kuchukiza mbele ya macho yangu

na usiendelee kutangatanga,

2ikiwa kwa kweli, kwa haki na kwa unyofu utaapa,

‘Kwa hakika kama vile Bwana aishivyo,’

ndipo mataifa yatakapobarikiwa naye

na katika yeye watajitukuza.”

3Hili ndilo asemalo Bwana kwa watu wa Yuda na kwa Yerusalemu:

“Vunjeni mabonge kwenye mashamba yenu,

wala msipande katikati ya miiba.

4Jitahirini katika Bwana,

tahirini mioyo yenu,

enyi wanaume wa Yuda

na watu wa Yerusalemu,

la sivyo ghadhabu yangu itatoka kwa nguvu

na kuwaka kama moto

kwa sababu ya uovu mliotenda,

ikiwaka pasipo wa kuizima.

Maafa Kutoka Kaskazini

5“Tangaza katika Yuda na upige mbiu katika Yerusalemu na kusema:

‘Piga tarumbeta katika nchi yote!’

Piga kelele na kusema:

‘Kusanyikeni pamoja!

Tukimbilie katika miji yenye maboma!’

6Onyesheni ishara ili kwenda Sayuni!

Kimbilieni usalama pasipo kuchelewa!

Kwa kuwa ninaleta maafa kutoka kaskazini,

maangamizi ya kutisha.”

7Simba ametoka nje ya pango lake,

mharabu wa mataifa amejipanga.

Ametoka mahali pake

ili aangamize nchi yenu.

Miji yenu itakuwa magofu

pasipo mtu wa kuishi humo.

8Hivyo vaeni nguo za magunia,

ombolezeni na kulia kwa huzuni,

kwa kuwa hasira kali ya Bwana

haijaondolewa kwetu.

9“Katika siku ile,” asema Bwana

“mfalme na maafisa watakata tamaa,

makuhani watafadhaika,

na manabii watashangazwa mno.”

10Ndipo niliposema, “Aa, Bwana Mwenyezi, umewadanganyaje kabisa watu hawa na Yerusalemu kwa kusema, ‘Mtakuwa na amani,’ wakati upanga uko kwenye koo zetu!”

11Wakati huo watu hawa na Yerusalemu wataambiwa, “Upepo wa moto kutoka miinuko iliyo kame katika jangwa unavuma kuelekea watu wangu, lakini sio kupepeta au kutakasa, 12upepo wenye nguvu sana kuliko wa kupepeta na kutakasa utakuja kwa amri yangu. Sasa natangaza hukumu zangu dhidi yao.”

13Tazama! Anakuja kama mawingu,

magari yake yanakuja kama upepo wa kisulisuli,

farasi wake wana mbio kuliko tai.

Ole wetu! Tunaangamia!

14Ee Yerusalemu, usafishe uovu kutoka moyoni mwako na uokolewe.

Utaendelea kuficha mawazo mapotovu mpaka lini?

15Sauti inatangaza kutoka Dani,

ikipiga mbiu ya maafa kutoka vilima vya Efraimu.

16“Waambie mataifa jambo hili,

piga mbiu hii dhidi ya Yerusalemu:

‘Jeshi la kuzingira linakuja kutoka nchi ya mbali,

likipiga kelele ya vita dhidi ya miji ya Yuda.

17Wamemzunguka kama watu walindao shamba,

kwa sababu amefanya uasi dhidi yangu,’ ”

asema Bwana.

18“Mwenendo wako na matendo yako mwenyewe

yameleta haya juu yako.

Hii ndiyo adhabu yako.

Tazama jinsi ilivyo chungu!

Tazama jinsi inavyochoma moyo!”

19Ee mtima wangu, mtima wangu!

Ninagaagaa kwa maumivu.

Ee maumivu makuu ya moyo wangu!

Moyo wangu umefadhaika ndani yangu,

siwezi kunyamaza.

Kwa sababu nimesikia sauti ya tarumbeta,

nimesikia kelele ya vita.

20Maafa baada ya maafa,

nchi yote imekuwa magofu.

Kwa ghafula mahema yangu yameangamizwa,

makazi yangu kwa muda mfupi.

21Hata lini nitaendelea kuona bendera ya vita

na kusikia sauti za tarumbeta?

22“Watu wangu ni wapumbavu,

hawanijui mimi.

Ni watoto wasio na akili,

hawana ufahamu.

Ni hodari kutenda mabaya,

hawajui kutenda yaliyo mema.”

23Niliitazama dunia,

nayo haikuwa na umbo tena ni tupu;

niliziangalia mbingu,

mianga ilikuwa imetoweka.

24Niliitazama milima, nayo ilikuwa ikitetemeka,

vilima vyote vilikuwa vikiyumbayumba.

25Nilitazama, wala watu hawakuwepo;

kila ndege wa angani alikuwa ameruka zake.

26Nilitazama, hata nchi iliyokuwa imestawi vizuri imekuwa jangwa,

miji yake yote ilikuwa magofu

mbele za Bwana,

mbele ya hasira yake kali.

27Hivi ndivyo Bwana asemavyo:

“Nchi yote itaharibiwa,

ingawa sitaiangamiza kabisa.

28Kwa hiyo dunia itaomboleza

na mbingu zilizo juu zitakuwa giza,

kwa sababu nimesema nami sitarudi nyuma,

nimeamua na wala sitageuka.”

29Kwa sauti ya wapanda farasi na wapiga upinde

kila mji unakimbia.

Baadhi wanakimbilia vichakani,

baadhi wanapanda juu ya miamba.

Miji yote imeachwa,

hakuna aishiye ndani yake.

30Unafanya nini, ewe uliyeharibiwa?

Kwa nini unajivika vazi jekundu

na kuvaa vito vya dhahabu?

Kwa nini unapaka macho yako rangi?

Unajipamba bure.

Wapenzi wako wanakudharau,

wanautafuta uhai wako.

31Nasikia kilio kama cha mwanamke

katika utungu wa kuzaa,

kilio cha uchungu kama cha anayemzaa

mtoto wake wa kwanza:

kilio cha Binti Sayuni akitweta ili aweze kupumua,

akiinua mikono yake, akisema,

“Ole wangu! Ninazimia;

maisha yangu yamekabidhiwa kwa wauaji.”