Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno) 2015

Yoeli 3:1-21

Mataifa Yahukumiwa

1“Katika siku hizo na wakati huo,

nitakaporejesha neema ya Yuda na Yerusalemu,

2nitayakusanya mataifa yote na kuyaleta

katika Bonde la Yehoshafati3:2 Yehoshafati maana yake Bwana huhukumu.

Hapo nitaingia kwenye hukumu dhidi yao

kuhusu urithi wangu, watu wangu Israeli,

kwa kuwa waliwatawanya watu wangu

miongoni mwa mataifa

na kuigawa nchi yangu.

3Wanawapigia kura watu wangu

na kuwauza wavulana ili kupata makahaba;

waliwauza wasichana

ili wapate kunywa mvinyo.

4“Sasa una nini dhidi yangu, ee Tiro na Sidoni, nanyi nchi zote za Ufilisti? Je, mnanilipiza kwa yale niliyoyafanya? Kama mnalipa, mimi nitalipiza juu ya vichwa vyenu kwa kasi na kwa haraka yale mliyoyatenda. 5Kwa kuwa mlichukua fedha na dhahabu yangu pia mkabeba hazina zangu nzuri sana mkapeleka kwenye mahekalu yenu. 6Mliwauza watu wa Yuda na Yerusalemu kwa Wayunani, ili kwamba mpate kuwapeleka mbali na nchi yao.

7“Tazama nitawaamsha kutoka zile sehemu mlizowauza, nami nitawalipiza juu ya vichwa vyenu kile mlichofanya. 8Nitawauza wana wenu na binti zenu kwa watu wa Yuda, nao watawauza kwa Waseba, taifa lililo mbali.” Bwana amesema.

9Tangazeni hili miongoni mwa mataifa:

Jiandaeni kwa vita!

Amsha askari!

Wanaume wote wapiganaji

wasogee karibu na kushambulia.

10Majembe yenu yafueni yawe panga

na miundu yenu ya kukatia iwe mikuki.

Aliye dhaifu na aseme,

“Mimi nina nguvu!”

11Njooni haraka, ninyi mataifa yote kutoka pande zote,

kusanyikeni huko.

Shusha wapiganaji wako, Ee Bwana!

12“Mataifa na yaamshwe;

na yasonge mbele kuelekea Bonde la Yehoshafati,

kwa kuwa nitaketi mahali pale

kuhukumu mataifa yote yaliyoko kila upande.

13Tia mundu,

kwa kuwa mavuno yamekomaa.

Njooni, mkanyage zabibu,

kwa kuwa shinikizo la kukamua zabibu limejaa

na mapipa yanafurika:

kwa kuwa uovu wao ni mkubwa!”

14Umati mkubwa, umati mkubwa

katika bonde la uamuzi!

Kwa kuwa siku ya Bwana ni karibu

katika bonde la uamuzi.

15Jua na mwezi vitatiwa giza,

na nyota hazitatoa mwanga wake tena.

16Bwana atanguruma kutoka Sayuni

na mshindo wa ngurumo kutoka Yerusalemu;

dunia na mbingu vitatikisika.

Lakini Bwana atakuwa kimbilio la watu wake,

ngome imara kwa ajili ya watu wa Israeli.

Baraka Kwa Watu Wa Mungu

17“Ndipo mtakapojua kwamba Mimi, Bwana Mungu wenu,

nakaa Sayuni, mlima wangu mtakatifu.

Yerusalemu utakuwa mtakatifu;

kamwe wageni hawatavamia tena.

18“Katika siku hiyo milima itadondosha divai mpya,

na vilima vitatiririka maziwa;

mabonde yote ya Yuda yatatiririka maji.

Chemchemi itatiririka kutoka kwenye nyumba ya Bwana

na kunywesha Bonde la Shitimu.3:18 Au: Bonde la Migunga.

19Lakini Misri itakuwa ukiwa,

Edomu itakuwa jangwa tupu,

kwa sababu ya jeuri waliofanya kwa watu wa Yuda,

ambao katika nchi yao

walimwaga damu isiyo na hatia.

20Yuda itakaliwa na watu milele

na Yerusalemu itadumu vizazi vyote.

21Hatia yao ya damu, ambayo sijasamehe,

nitasamehe.”

Bwana anakaa Sayuni!