Neno Alifanyika Mwili
1Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.
3Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. 4Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. 5Nuru hungʼaa gizani nalo giza halikuishinda.
6Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. 7Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kwa kupitia kwake watu wote waweze kuamini. 8Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru. 9Kwamba nuru halisi, imwangaziayo kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni.
10Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. 11Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. 12Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 13Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.
14Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.
15Yohana alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’ ” 16Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema. 17Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Mose, lakini neema na kweli imekuja kupitia Yesu Kristo. 18Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba ndiye ambaye amemdhihirisha.
Ushuhuda Wa Yohana Mbatizaji
(Mathayo 3:1-12; Marko 1:1-8; Luka 3:1-18)
19Huu ndio ushuhuda wa Yohana wakati Wayahudi walipowatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumuuliza, “Wewe ni nani?” 20Yohana alikiri waziwazi pasipo kuficha akasema, “Mimi si Kristo.”1:20 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.
21Wakamuuliza, “Wewe ni nani basi? Je, wewe ni Eliya?”
Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.”
“Je, wewe ni yule Nabii?”
Akajibu, “Hapana.”
22Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?”
23Akawajibu kwa maneno ya nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Yanyoosheni mapito ya Bwana.’ ”
24Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo 25wakamuuliza, “Kama wewe si Kristo, wala si Eliya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza?”
26Yohana akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji,1:26 Hapa tafsiri zingine zinasema ndani ya maji. lakini katikati yenu yupo mtu msiyemjua. 27Yeye ajaye baada yangu, sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.”
28Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ngʼambo ya Mto Yordani, mahali Yohana alipokuwa akibatiza.
Yesu Mwana-Kondoo Wa Mungu
29Siku iliyofuata, Yohana alimwona Yesu akimjia akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu! 30Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’ 31Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.”
32Kisha Yohana akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake. 33Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.’ 34Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.”
Wanafunzi Wa Kwanza Wa Yesu
35Siku iliyofuata, Yohana alikuwa huko tena pamoja na wanafunzi wake wawili. 36Alipomwona Yesu akipita, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!”
37Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yohana akisema haya, wakamfuata Yesu. 38Yesu akageuka, akawaona wakimfuata akawauliza, “Mnataka nini?”
Wakamwambia, “Rabi,” (maana yake Mwalimu), “Unaishi wapi?”
39Yesu akawajibu, “Njooni, nanyi mtapaona!”
Hivyo wakaenda na kupaona mahali alipokuwa anaishi, wakakaa naye siku ile, kwa kuwa ilikuwa yapata saa kumi.
40Andrea nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia yale Yohana aliyokuwa amesema, naye ndiye alimfuata Yesu. 41Kitu cha kwanza Andrea alichofanya ni kumtafuta Simoni nduguye na kumwambia, “Tumemwona Masiya” (yaani, Kristo). 42Naye akamleta kwa Yesu.
Yesu akamwangalia na kusema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana. Utaitwa Kefa” (ambalo limetafsiriwa Petro1:42 Petro kwa Kiyunani au Kefa kwa Kiaramu; maana yake ni Kipande cha mwamba.).
Yesu Awaita Filipo Na Nathanaeli
43Siku iliyofuata Yesu aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
44Basi Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji alikotoka Andrea na Petro. 45Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Mose aliandika habari zake katika Sheria na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani, Yesu wa Nazareti, mwana wa Yosefu.”
46Nathanaeli akauliza, “Nazareti! Je, kitu chochote chema chaweza kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.”
47Yesu alipomwona Nathanaeli anakaribia, akanena habari zake akasema, “Tazama huyu ni Mwisraeli kweli kweli; hana hila ndani yake.”
48Nathanaeli akamuuliza, “Umenifahamuje?”
Yesu akamjibu, “Nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.”
49Nathanaeli akamwambia, “Rabi, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!”
50Yesu akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nilikuambia nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu zaidi kuliko hilo.” 51Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”