Yesu Akamatwa
(Mathayo 26:47-56; Marko 14:43-50; Luka 22:47-53)
1Yesu alipomaliza kuomba, akaondoka na wanafunzi wake wakavuka Bonde la Kidroni. Upande wa pili palikuwa na bustani, yeye na wanafunzi wake wakaingia humo.
2Basi Yuda, yule aliyemsaliti alipafahamu mahali hapo kwani Yesu alikuwa akikutana humo na wanafunzi wake mara kwa mara. 3Hivyo Yuda akaja bustanini. Aliongoza kikosi cha askari wa Kirumi, na baadhi ya maafisa kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Nao walikuwa wamechukua taa, mienge na silaha.
4Yesu akijua yale yote yatakayompata, akajitokeza mbele yao akawauliza, “Mnamtafuta nani?”
5Wao wakamjibu, “Yesu wa Nazareti.”
Yesu akawajibu, “Mimi ndiye.” Yuda, yule aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. 6Yesu alipowaambia, “Mimi ndiye,” walirudi nyuma na kuanguka chini!
7Akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?”
Nao wakamjibu, “Yesu wa Nazareti.”
8Yesu akawaambia, “Nimekwisha kuwaambia kuwa, mimi ndiye; kwa hiyo kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa watu waende zao.” 9Hii ilikuwa ili litimie lile neno alilosema, “Sikumpoteza hata mmoja miongoni mwa wale ulionipa.”
10Simoni Petro, aliyekuwa na upanga, akaufuta na kumkata sikio la kuume mtumishi wa kuhani mkuu. Jina la mtumishi huyo aliitwa Malko.
11Yesu akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako kwenye ala yake. Je, hainipasi kukinywea kikombe alichonipa Baba?”
Yesu Mbele Ya Kuhani Mkuu
12Hivyo wale askari, wakiwa pamoja na majemadari wao na maafisa wa Wayahudi, wakamkamata Yesu na kumfunga. 13Kwanza wakampeleka kwa Anasi, mkwewe Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu mwaka ule. 14Kayafa ndiye alikuwa amewashauri Wayahudi kwamba imempasa mtu mmoja kufa kwa ajili ya watu.
Petro Anamkana Yesu
(Mathayo 26:69-70; Marko 14:55-64; Luka 22:66-71)
15Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walikuwa wakimfuata Yesu. Huyu mwanafunzi mwingine alikuwa anafahamika kwa kuhani mkuu, hivyo aliingia ndani ya ukumbi pamoja na Yesu. 16Lakini Petro alisimama nje karibu na lango, ndipo yule mwanafunzi mwingine, aliyejulikana na kuhani mkuu, akazungumza na msichana aliyekuwa analinda lango, akamruhusu Petro aingie ndani.
17Yule msichana akamuuliza Petro, “Je, wewe pia si mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?”
Petro akajibu, “Sio mimi.”
18Wale watumishi na askari walikuwa wamesimama wakiota moto wa makaa kwa sababu palikuwa na baridi, Petro naye alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto.
Kuhani Mkuu Amhoji Yesu
19Wakati huo kuhani mkuu akawa anamuuliza Yesu kuhusu wanafunzi wake na mafundisho yake.
20Yesu akamjibu, “Nimekuwa nikizungumza waziwazi mbele ya watu wote. Siku zote nimefundisha katika masinagogi na Hekaluni, mahali ambapo Wayahudi wote hukusanyika. Sikusema jambo lolote kwa siri. 21Mbona unaniuliza mimi maswali? Waulize wale walionisikia yale niliyowaambia. Wao wanajua niliyosema.”
22Alipomaliza kusema hayo, mmoja wa askari aliyekuwa amesimama karibu naye, akampiga Yesu kofi usoni, kisha akasema, “Je, hivyo ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?”
23Yesu akamjibu akasema, “Kama nimesema jambo baya, shuhudia huo ubaya niliousema. Lakini kama nimesema yaliyo kweli, mbona umenipiga?” 24Ndipo Anasi akampeleka Yesu kwa kuhani mkuu Kayafa, akiwa bado amefungwa.
Petro Amkana Yesu Tena
(Mathayo 26:71-75; Marko 14:69-72; Luka 22:58-62)
25Wakati huo Simoni Petro alikuwa amesimama akiota moto. Baadhi ya wale waliokuwepo wakamuuliza, “Je, wewe si mmoja wa wanafunzi wake?”
Petro akakana, akasema, “Sio mimi.”
26Mmoja wa watumishi wa kuhani mkuu, ndugu yake yule mtu ambaye Petro alikuwa amemkata sikio, akamuuliza, “Je, mimi sikukuona kule bustanini ukiwa na Yesu?” 27Kwa mara nyingine tena Petro akakana, naye jogoo akawika wakati huo huo.
Yesu Apelekwa Kwa Pilato
(Mathayo 27:1-2, 11-14; Marko 15:1-5; Luka 23:1-5)
28Ndipo Wayahudi wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa na kumpeleka kwenye jumba la kifalme la mtawala wa Kirumi.18:28 Jumba la mfalme la mtawala wa Kirumi lilikuwa linaitwa Praitorio. Wakati huo ilikuwa ni alfajiri, ili kuepuka kuwa najisi kwa taratibu za ibada, Wayahudi hawakuingia ndani kwa sababu ya sheria za Kiyahudi. Wangehesabiwa kuwa najisi kama wangeingia nyumbani mwa mtu asiye Myahudi na wasingeruhusiwa kushiriki katika Sikukuu ya Pasaka. 29Hivyo Pilato akatoka nje walikokuwa akawauliza, “Mmeleta mashtaka gani kumhusu mtu huyu?”
30Wao wakamjibu, “Kama huyu mtu hakuwa mhalifu tusingemleta kwako.”
31Pilato akawaambia, “Basi mchukueni ninyi mkamhukumu kwa kufuata sheria zenu.”
Wayahudi wakamjibu, “Sisi haturuhusiwi kutoa hukumu ya kifo kwa mtu yeyote.” 32Walisema hivyo ili yale maneno aliyosema Yesu kuhusu kifo atakachokufa yapate kutimia.
33Kwa hiyo Pilato akaingia ndani ya jumba la kifalme, akamwita Yesu, akamuuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”
34Yesu akamjibu, “Je, unauliza swali hili kutokana na mawazo yako mwenyewe, au uliambiwa na watu kunihusu mimi?”
35Pilato akamjibu, “Mimi si Myahudi, ama sivyo? Taifa lako mwenyewe na viongozi wa makuhani wamekukabidhi kwangu. Umefanya kosa gani?”
36Yesu akajibu, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, wafuasi wangu wangenipigania ili nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini kama ilivyo, ufalme wangu hautoki hapa ulimwenguni.”
37Pilato akamuuliza, “Kwa hiyo wewe ni mfalme?” Yesu akajibu, “Wewe wasema kwamba mimi ni mfalme. Kwa kusudi hili nilizaliwa, na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Mtu yeyote aliye wa kweli husikia sauti yangu.”
38Pilato akamuuliza Yesu, “Kweli ni nini?” Baada ya kusema haya Pilato akaenda nje tena akawaambia wale viongozi wa Wayahudi waliomshtaki Yesu, “Sioni kosa lolote alilotenda mtu huyu. 39Lakini ninyi mna desturi yenu kwamba wakati wa Pasaka nimwachie huru mfungwa mmoja mnayemtaka. Je, mnataka niwafungulie huyu ‘Mfalme wa Wayahudi’?”
40Wao wakapiga kelele wakisema, “Si huyu mtu, bali tufungulie Baraba!” Yule Baraba alikuwa mnyangʼanyi.