Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno) 2015

Zaburi 145:1-21

Zaburi 145145:1 Zaburi hii imetungwa kila mstari (ikiwa ni pamoja na 13b) ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.

Wimbo Wa Kusifu Ukuu Na Wema Wa Mungu

Wimbo wa Sifa. Wa Daudi.

1Nitakutukuza wewe, Mungu wangu Mfalme,

nitalisifu jina lako milele na milele.

2Kila siku nitakusifu

na kulitukuza jina lako milele na milele.

3Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,

ukuu wake haupimiki.

4Kizazi kimoja kitasifia kazi zako kwa kizazi kingine,

watasimulia matendo yako makuu.

5Watasema juu ya utukufu wa fahari ya ukuu wako,

nami nitatafakari juu ya kazi zako za ajabu.

6Watasimulia uwezo wa kazi zako za kutisha,

nami nitatangaza matendo yako makuu.

7Wataadhimisha wema wako mwingi,

na wataimba kwa shangwe juu ya haki yako.

8Bwana ni mwenye neema na mwingi wa huruma,

si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo.

9Bwana ni mwema kwa wote,

ana huruma kwa vyote alivyovifanya.

10Ee Bwana, vyote ulivyovifanya vitakusifu,

watakatifu wako watakutukuza.

11Watasimulia utukufu wa ufalme wako

na kusema juu ya ukuu wako,

12ili watu wote wajue matendo yako makuu

na utukufu wa fahari ya ufalme wako.

13Ufalme wako ni ufalme wa milele,

mamlaka yako hudumu vizazi vyote.

Bwana ni mwaminifu kwa ahadi zake zote

na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.

14Bwana huwategemeza wote waangukao,

na huwainua wote waliolemewa na mizigo yao.

15Macho yao wote yanakutazama wewe,

nawe huwapa chakula chao wakati wake.

16Waufumbua mkono wako,

watosheleza haja ya kila kitu kilicho hai.

17Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,

na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya.

18Bwana yu karibu na wote wamwitao,

karibu na wote wamwitao kwa uaminifu.

19Huwatimizia wamchao matakwa yao,

husikia kilio chao na kuwaokoa.

20Bwana huwalinda wote wampendao,

bali waovu wote atawaangamiza.

21Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana.

Kila kiumbe na kilisifu jina lake takatifu

milele na milele.